Skip to content
Nelum
Laws of Tanzania

Taarifa kwa Umma: Mrejesho wa Ukaguzi wa Miradi ya Msaada wa Kiufundi kwa Wachimbaji Wadogo wa Madini

Text as of 2026-09-29

Public law and official guidance, published as research. Not legal, tax or financial advice.

About this law

Kind
Other
Number
Mining Commission press release (Word file TAARIFA_KWA_UMMA_-ES.doc)
Issued by
Mining Commission, Dodoma
Country
Tanzania

Where to read it

Text

The law's own text, section by section, as held. Each section has its own link.

  1. TAARIFA KWA UMMA MREJESHO WA UKAGUZI WA MIRADI YA MSAADA WA KIUFUNDI KWA WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI Ndugu Waandishi wa Habari, Tarehe 27 Aprili 2026 wakati wa hotuba ya uwasilishaji wa bajeti ya Wizara ya Madini ya mwaka 2026/2027, Waziri wa Madini Mhe. Anthony Peter Mavunde, aliielekeza Tume ya Madini kufanya ukaguzi wa miradi yote ya uchimbaji madini kupitia leseni ndogo za uchimbaji wa madini zenye mikataba ya Msaada wa Kiufundi (TSA) ili kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikataba hiyo kwa kuzingatia Sheria ya Madini, Sura 123. Ndugu Waandishi wa Habari, Kufuatia maelekezo hayo, Tume ya Madini imefanya ukaguzi wa miradi yote ya uchimbaji mdogo wa madini yenye Mikataba ya Msaada wa Kiufundi ili kuhakiki utendaji kazi wa miradi hiyo, uzingatiaji wa masharti ya mikataba pamoja na matakwa ya Sheria na Kanuni zake kwa wamiliki wa leseni pamoja na watoa msaada wa kiufundi. Ndugu Waandishi wa Habari, Jumla ya miradi 128 ilikaguliwa. Kati ya hiyo, miradi 42 ilibainika kuwa haifanyi kazi. Miradi 86 ilibainika kuwa inafanya kazi, lakini ina changamoto mbalimbali katika utekelezaji na uzingatiaji wa masharti ya Mikataba ya Msaada wa Kiufundi. Miongoni mwa changamoto zilizobainika katika miradi inayofanya kazi ni pamoja na kutotekeleza ipasavyo mipango inayotakiwa kisheria, ikiwemo Mpango wa Usimamizi wa Mazingira ulioidhinishwa, Mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), Mpango wa Uhawilishaji wa Teknolojia (Technology Transfer Plan), Mpango wa Uchimbaji (Mining Plan), pamoja na Mpango wa Ufunguaji wa Mgodi (Mine Closure Plan). HATUA ZINAZOCHUKULIWA Ndugu Waandishi wa Habari, Kutokana na matokeo ya ukaguzi huo, Tume ya Madini imeanza kuchukua hatua mbalimbali za kiusimamizi na kisheria. Kwa miradi 42 iliyobainika kuwa haifanyi kazi, Hati za Makosa za siku 30 zimetolewa kwa wamiliki husika na kama hakutakuwa na mrejesho chanya ndani ya muda uliotolewa, taratibu za kisheria zitafuata ikiwemo kufuta ridhaa ya utoaji wa Msaada wa Kiufundi. Aidha, Kwa miradi 86 inayofanya kazi lakini ina mapungufu, wamiliki na wawezeshaji wa Msaada wa Kiufundi wameelekezwa kurekebisha mapungufu yao kwa mujibu wa Kanuni za Msaada wa Kiufundi kwa Wamiliki wa Leseni Ndogo za Uchimbaji Madini za Mwaka 2025, ndani ya siku 30. Endapo wahusika watashindwa kutekeleza matakwa yaliyowekwa ndani ya muda huo, hatua zaidi za kisheria zitachukuliwa, ikiwemo kufuta ridhaa ya Msaada wa Kiufundi. KUIMARISHA UKAGUZI NA UFUATILIAJI Ndugu Waandishi wa Habari, Nitumie fursa hii kuwakumbusha wanufaika wa Misaada ya Kiufundi kuwa, Tume ya Madini itaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika miradi ya Msaada wa Kiufundi ili kuhakikisha kuwa miradi yote inatekelezwa kwa mujibu wa sheria, kanuni, na masharti ya ridhaa iliyotolewa. Tume itaendelea kuchukua hatua za kisheria ikiwemo kufuta ridhaa ya Misaada ya Kiufundi pale itakapobainika inakiuka matakwa ya Sheria ya Madini na Kanuni zake. Aidha, niwakumbushe pia wanufaika wa Misaada ya Kiufundi na wachimbaji madini wote nchini kuzingatia masuala ya utunzaji wa mazingira, usalama pamoja na afya kazini wakati wote na hususan katika kipindi hiki ambacho tumetahadharishwa kutokea kwa mvua za El Nino hivi karibuni. Ndugu Waandishi wa Habari, Namalizia kwa kusisitiza kuwa, Msaada wa Kiufundi umewekwa kisheria kuwa nyenzo ya kuwawezesha wachimbaji wadogo wasiokuwa na uwezo kuendeleza maeneo yao, kuongeza tija na uzalishaji pamoja na kuhamisha mbinu na teknolojia mbalimbali katika uchimbaji na uchenjuaji wa madini ili kumwezesha mchimbaji mdogo kukua. Hivyo, wamiliki wote wa leseni za uchimbaji mdogo mlioingia makubaliano ya Msaada wa Kiufundi, hakikisheni mnatendea haki mikataba yenu kwa manufaa yenu na taifa kwa ujumla. Asanteni kwa kunisikiliza. TUME YA MADINI Dodoma Agosti 2026

Taarifa kwa Umma: Mrejesho wa Ukaguzi wa Miradi ya Msaada wa Kiufundi kwa Wachimbaji Wadogo wa Madini · Nelum